Daniel 7:14-27

14 aAkapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu; nao watu wa kabila zote, mataifa, na watu wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.

Tafsiri Ya Ndoto

15 b“Mimi, Danieli, nilipata mahangaiko rohoni, nayo maono yale yaliyopita ndani ya mawazo yangu yalinisumbua. 16 cNikamkaribia mmoja wa wale waliosimama pale na kumuuliza maana halisi ya haya yote.

“Basi akaniambia na kunipa tafsiri ya vitu hivi:
17‘Hao wanyama wanne wakubwa ni falme nne zitakazoinuka duniani. 18 dLakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele: naam, milele na milele.’

19“Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, ambaye alikuwa tofauti na wale wengine wote, tena wa kutisha sana, na meno yake ya chuma na makucha ya shaba: mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chochote kilichosalia. 20 ePia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake, na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho zaidi kuliko zile nyingine, na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno. 21 fNilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda, 22 gmpaka huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipoumiliki ufalme.

23 h“Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote, nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda. 24 iZile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu. 25 jAtanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwaonea watakatifu wake, huku akijaribu kubadili majira na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati.
Wakati, nyakati mbili, na nusu wakati maana yake ni mwaka mmoja, miaka miwili, na nusu mwaka, yaani miaka mitatu na nusu.


26 l“ ‘Lakini mahakama itakaa kuhukumu, nayo mamlaka yake yataondolewa na kuangamizwa kabisa milele. 27 mNdipo ufalme, mamlaka na ukuu wa falme chini ya mbingu yote utakabidhiwa kwa watakatifu, watu wa Yeye Aliye Juu Sana. Ufalme wake utakuwa ufalme wa milele, nao watawala wote watamwabudu na kumtii yeye.’

Copyright information for SwhNEN